Biblia mwaka mmoja


Februari 21


Matthayo 21:1-22
1. Hata walipokaribia Yerusalemu, na kufika Bethfage, katika mlima wa Mizeituni, ndipo Yesu alipotuma wanafunzi wawili akiwaambia,
2. Enendeni mpaka kijiji kile kinachowakabili, na mara mtaona punda amefungwa, na mwana-punda pamoja naye; wafungueni mniletee.
3. Na kama mtu akiwaambia neno, semeni, Bwana anawahitaji; na mara huyo atawapeleka.
4. Haya yote yamekuwa, ili litimie neno lililonenwa na nabii, akisema,
5. Mwambieni binti Sayuni Tazama, mfalme wako anakuja kwako, Mpole, naye amepanda punda, Na mwana-punda, mtoto wa punda.
6. Wale wanafunzi wakaenda zao, wakafanya kama Yesu alivyowaamuru,
7. wakamleta yule punda na mwana-punda, wakaweka nguo zao juu yao, naye akaketi juu yake.
8. Watu wengi katika ule mkutano wakatandaza nguo zao njiani; na wengine wakakata matawi ya miti, wakayatandaza njiani.
9. Na makutano waliotangulia, na wale waliofuata, wakapaza sauti, wakisema, Hosana, Mwana wa Daudi; ndiye mbarikiwa, yeye ajaye kwa jina la Bwana; Hosana juu mbinguni.
10. Hata alipoingia Yerusalemu, mji wote ukataharuki, watu wakisema, Ni nani huyu?
11. Makutano wakasema, Huyu ni yule nabii, Yesu, wa Nazareti ya Galilaya.
12. Yesu akaingia ndani ya hekalu, akawafukuza wote waliokuwa wakiuza na kununua hekaluni, akazipindua meza za wabadili fedha, na viti vyao waliokuwa wakiuza njiwa;
13. akawaambia, Imeandikwa, Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala; bali ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyang'anyi.
14. Na vipofu na viwete wakamwendea mle hekaluni, akawaponya.
15. Lakini wakuu wa makuhani na waandishi walipoyaona maajabu aliyoyafanya, na watoto waliopaza sauti zao hekaluni, wakisema, Hosana, Mwana wa Daudi! Walikasirika,
16. wakamwambia, Wasikia hawa wasemavyo? Yesu akawaambia, Naam; hamkupata kusoma, Kwa vinywa vya watoto wachanga na wanyonyao umekamilisha sifa?
17. Akawaacha, akatoka nje ya mji mpaka Bethania, akalala huko.
18. Hata asubuhi alipokuwa akienda mjini, aliona njaa.
19. Akaona mtini mmoja kando ya njia, akauendea, asione kitu juu yake ila majani tu; akauambia, Yasipatikane matunda kwako tangu leo hata milele. Mtini ukanyauka mara.
20. Wanafunzi walipoona, walistaajabu, wakisema, Jinsi gani mtini umenyauka mara?
21. Yesu akajibu, akawaambia, Amin, nawaambia Mkiwa na imani, msipokuwa na shaka, mtafanya si hilo la mtini tu, lakini hata mkiuambia mlima huu, Ng'oka, ukatupwe baharini, litatendeka.
22. Na yo yote mtakayoyaomba katika sala mkiamini, mtapokea.