Bible Selection
Agano la Kale
Agano Jipya
Kiswahili Biblia 1997

Methali 10

1

Mwana mwenye hekima humfurahisha babaye; Bali mwana mpumbavu ni mzigo wa mamaye.

2

Hazina za uovu hazifaidii kitu; Bali haki huokoa na mauti.

3

Bwana hataiacha nafsi ya mwenye haki ife na njaa; Bali tamaa ya mtu mwovu huisukumia mbali.

4

Atendaye mambo kwa mkono mlegevu huwa maskini; Bali mkono wake aliye na bidii hutajirisha.

5

Akusanyaye wakati wa hari ni mwana mwenye hekima; Bali asinziaye wakati wa mavuno ni mwana mwenye kuaibisha.

6

Baraka humkalia mwenye haki kichwani; Bali jeuri hufunika kinywa chake mtu mwovu.

7

Kuwakumbuka wenye haki huwa na baraka; Bali jina la mtu mwovu litaoza.

8

Aliye na akili moyoni mwake atapokea agizo; Bali mpumbavu mwenye maneno mengi ataanguka.

9

Aendaye kwa unyofu huenda salama; Bali apotoshaye njia zake atajulikana.

10

Akonyezaye kwa jicho huleta masikitiko; Bali mpumbavu mwenye maneno mengi ataanguka.

11

Kinywa chake mwenye haki ni chemchemi ya uzima; Bali jeuri hufunika kinywa chake mtu mwovu,

12

Kuchukiana huondokesha fitina; Bali kupendana husitiri makosa yote.

13

Hekima hupatikana midomoni mwa mwenye ufahamu; Bali fimbo hufaa kwa mgongo wake asiye na ufahamu.

14

Watu wenye akili huweka akiba ya maarifa; Bali kinywa cha mpumbavu ni uangamivu ulio karibu.

15

Mali ya mtu tajiri ni mji wake wa nguvu; Uangamivu wa maskini ni umaskini wao.

16

Kazi yake mwenye haki huuelekea uzima; Mazao ya wabaya huuelekea dhambi.

17

Akubaliye kurudiwa huwa katika njia ya uzima; Bali yeye aachaye maonyo hukosa.

18

Yeye afichaye chuki ana midomo ya uongo, Na yeye asingiziaye ni mpumbavu.

19

Katika wingi wa maneno hapakosi kuwa na maovu; Bali yeye azuiaye midomo yake hufanya akili.

20

Ulimi wa mwenye haki ni kama fedha teule; Moyo wa mtu mbaya haufai kitu.

21

Midomo ya mwenye haki hulisha watu wengi; Bali wapumbavu hufa kwa kuwa hawana ufahamu.

22

Baraka ya Bwana hutajirisha, Wala hachanganyi huzuni nayo.

23

Kwa mpumbavu kutenda maovu ni kama mchezo; Bali mtu mwenye ufahamu ana hekima.

24

Aogopacho mtu asiye haki ndicho kitakachomjilia; Na wenye haki watapewa matakwa yao.

25

Kisulisuli kikiisha pita asiye haki hayuko tena; Bali mwenye haki ni msingi wa milele.

26

Kama siki menoni, na kama moshi machoni, Ndivyo alivyo mtu mvivu kwao wamtumao.

27

Kumcha Bwana kwaongeza siku za mtu; Bali miaka yao wasio haki itapunguzwa.

28

Matumaini yao wenye haki yatakuwa furaha; Bali kutaraji kwao wasio haki kutapotea.

29

Njia ya Bwana ni kimbilio lake mtu mkamilifu; Bali ni uharibifu kwao watendao maovu.

30

Mwenye haki hataondolewa milele; Bali wasio haki hawatakaa katika nchi.

31

Kinywa cha mwenye haki hutoa hekima; Bali ulimi wa ukaidi utakatiliwa mbali.

32

Midomo ya mwenye haki huyajua yatakayokubaliwa; Bali kinywa chao wasio haki hunena ukaidi.

Swahili Bible 1997
1952, 1997: Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya. All rights reserved.