Bible Selection
Agano la Kale
Agano Jipya
Kiswahili Biblia 1997

Zaburi 75

1

Ee Mungu, twakushukuru. Twakushukuru kwa kuwa Jina lako li karibu; Watu huyasimulia matendo yako ya ajabu.

2

Nitakapoufikia wakati ulioamriwa, Mimi nitahukumu hukumu za haki.

3

Ingawa dunia na wote wakaao humo wataharuki, Mimi mwenyewe nimezisimamisha nguzo zake.

4

Naliwaambia waliojivuna, Msijivune; Na wasio haki, Msiiinue pembe.

5

Msiiinue pembe yenu juu, Wala msinene kwa shingo ya kiburi.

6

Maana siko mashariki wala magharibi, Wala nyikani itokako heshima.

7

Bali Mungu ndiye ahukumuye; Humdhili huyu na kumwinua huyu.

8

Maana mkononi mwa Bwana mna kikombe, Na mvinyo yake inatoka povu; Kumejaa machanganyiko; Naye huyamimina. Na sira zake wasio haki wa dunia Watazifyonza na kuzinywa.

9

Bali mimi nitatangaza matendo yako milele, Nitamwimbia Mungu wa Yakobo.

10

Pembe zote za wasio haki nitazikata, Na pembe za mwenye haki zitainuka.

Swahili Bible 1997
1952, 1997: Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya. All rights reserved.